Close

Close

Aina Za Uchafu Ukeni

Kuna aina nyingi za uchafu ukeni. Aina zifuatazo zimegawanywa kwa kulingana na rangi na kiwango cha utokaji wake. Utaona kwamba aina zingine za uchafu ni salama na uchafu mwingine siyo salama, unaashiria kuwepo kwa ugonjwa

Uchafu Mweupe Ukeni

Kutokwa na uchafu mweupe hasa mwanzoni mwa hedhi au mwishoni mwa hedhi ni jambo la kawaida. Hata hivo kama uchafu huu unaambatana na muwasho na ni mzito sana kama maziwa ujue siyo kawaida na inahitaji upate vipimo na tiba hospitali kwani ni kiashiria cha fangasi ukeni.

Uchafu Mwepesi Kama Maji

Uchafu mwepesi kama maji ni kawaida kabisa. Unaweza kupata uchafu huu muda wowote katika mzunguko wako na hasa baada ya kufanya mazoezi.

Uchafu Mwepesi Unaovutika

Ukiona uteute mwepesi na unavutika kama ute wa yai basi ujue upo kwenye ovulation, yaani siku za hatari na yai limepevuka tayari kwa kurutubishwa. Uteute huu ni wa kawaida.

Uchafu wa Brown Unaoambatana na Damudamu.

Kama unapata uteute huu kabla ya hedhi na ulifanya tendo bila kinga basi kuna uwezekano ukawa umeshika mimba. Kama uchafu huu unatoka wakati mimba yako bado ni changa basi yaweza kuashiria kwamba mimba inaharibika unatakiwa kuwahi hospitali haraka.

Kwa kesi chache sana uchafu wa brown wenye damu damu ni kiashiria cha saratani ya shingo ya kizazi ama pia uvimbe kwenye kizazi(fibroids) ama uvimbe mwingine kwenye kizazi. Ndio maana ni muhimu sana kufanya utrasound kucheki hali ya kizazi endapo utaona dalili zisizo za kawaida kama hizi.

Uchafu Wa Njano au Kijani

Kama unapata uchafu wa kijani au njano unaoambatana na harufi mbaya siyo jambo la kawaida. Uchafu wa namna hii ni kiashiria kwamba kuna maambukizi ya ugonjwa wa zinaa. Inahitaji uende hospitali haraka kupata vipimo pamoja na tiba.