Close

Close

KISONONO (GONORRHEA)

Kisonono ni ugonjwa kati ya magonjwa ya zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Neisseria gonorrhoeae.

Bakteria ambao hukuwa na kuzaliana kwa haraka katika sehemu zenye unyevunyevu na joto mwilini. Kama kwenye shingo ya kizazi kwa wanawake (cervix), mirija ya kupitisha mkojo au shahawa (urethra), mdomoni na kwenye puru (rectum).

Dalili Za Kisonono Kwa Mwanaume

  1. Kuhisi kama kichomi wakati wa kukojoa (burning sensation)
  2. Kutokwa na majimaji ya njano au meupe au ya kijani kutoka kwenye uume yanayoambatana na maumivu makali sana
  3. Wakati mwengine maumivu au kuvimba kwa korodani (swollen testicles) Maambukizi yakiwa kwenye puru (rectum) huambatana na maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa.

Kuwashwa sehemu za haja kubwa, na hata haja kubwa inaweza kutoka ikiambatana na damu. Hii inatokea kwa wanaume na wanawake.

Dalili kwa wanawake:

Huwa si nyingi lakini wanawake wengi hawaonyeshi dalili zozote. Hizi dalili ni kama:

  1. Maumivu au kuhisi kama kichomi wakati wa kukojoa
  2. Kuongezeka kwa kutoka majimaji kutoka kwenye tupu ya mwanamke ambayo ni ya njano au yamechanganyika na damu
  3. Kutokwa na damu kabla ya hedhi kufika
  4. Kutokwa na damu baada ya kujamiana au baada ya tendo la ndoa
  5. Kichefuchefu, Homa (fever), Kutapika

Vipimo Vya Ugonjwa Wa Kisonono

1. Swab for culture

Kipimo hiki hufanyika maabara kwa kupandikiza bakteria baada ya kufuta sehemu za siri kwa kutumia swab ili kuona kama kuna bakteria wanaosababisha gono.

2. Polymerase Chain Reaction (PCR)

Kipimo cha kuangalia vina saba (DNA) ya bakteria, ni ghali sana.

Tiba Ya Ugonjwa Wa Kisonono Ni Nini?

Tiba ya gono inahusisha na tiba ya ugonjwa wa Chlamydia kwani mara nyingi magonjwa haya huambatana kwa pamoja.Tiba hutegemea na umri wa mgonjwa na kama mtu ni mjamzito au la.

Tiba ya gono ambayo sio sugu iliyo kwenye shingo ya kizazi (cervix), urethra na puru, dawa zinazotumika ni aina za cephalosporin dozi moja pamoja na dawa za aina ya macrolide antibiotics (mfano azithromycin) na za jamii ya penicillin (mfano doxycyclin) ili kutibu ugonjwa wa chlamydia.

Mara nyingi kwa wale chini ya miaka 18 na wanawake wajawazito, hutibiwa kwa kuchomwa sindano.

Fuata ushauri wa daktari kabla ya kutumia dawa hizi kwani dawa nyingi zina madhara kwa wajawazito (mfano doxycyclin).

Ushauri nasaha hutolewa kwa wapenzi wote wawili na ni vizuri wapenzi wote wawili kutibiwa hata kama mmoja hana dalili za ugonjwa huu.

Madhara Ya Ugonjwa Wa Kisonono Ni:

  1. Kutoweza kuzaa kwa mwanamke (tasa) au kutoweza kutungisha mimba kwa mwanamume (infertility)
  2. Huweza kuathiri moyo (heart valves), ubongo,ngozi nk ambayo ni hatari sana kwa mtu yoyote
  3. Madhara kwenye sehemu za maungio au jointi (joint inflammation)
  4. Kwa wanawake wale ambao hawajatibiwa wanaweza kupata ugonjwa wa PID (Pelvic Inflammatory Disease) ambao huongeza asilimia ya mwanamke kuwa tasa
  5. Wale wanawake ambao ni wajawazito na wameambukizwa gono wako kwenye hatari ya mimba kutoka au kuzaa mapema kabla mimba haijatimiza umri wake (preterm labor)
  6. Kwa wale wanaoambukizwa gono kipindi cha kukaribia kujifungua, wanaweza kuwaambukiza watoto wao na hivyo watoto kupata ugonjwa wa uti wa mgongo (meningitis), kuwa kipofu (blindness), homa ya mapafu (pneumonia) na ugonjwa wa mifupa (septic arthritis)

Kinga Ya Kisonono

  1. Kutumia kondomu wakati wa kujamiana
  2. Kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu
  3. Kwa wanawake wajawazito Hakikisha unahudhuria kliniki mapema ili upate kuchunguzwa na kupatiwa tiba muafaka kama utagundulika na ugonjwa wa gono au ugonjwa mwengine wowote
  4. Wanawake wajawazito wanashauriwa kujifungulia hospitali ili kama mtoto ameathirika na gono apate matibabu ya haraka baada ya kuzaliwa kuepusha kuwa kipofu

Kumbuka ya kwamba hakuna kitu kama ngono salama kwani huwezi kujua kama wewe au mwenzako wakati wa kujamiana ameathirika au la, au una michibuko au umekatika kwenye ngozi au la kwani michibuko mengine inaweza isionekane au kugundulika kwa urahisi.

Njia pekee na nzuri ni kuacha au kujikinga na vitendo vya ngono. Mtu aliyepata gono awali anaweza pata tena kama hatapata tiba sahihi.