Wanawake wengi wanapenda kutumia manukato na vitu vingine kama sabuni zenye kemikali kwa ajili ya kunuki. Pia, wanawake wamekuwa wakipenda usafi wao binafsi, wakitumia vitu ambavyo baadhi yake ni hatari. Wapo baadhi ya wanawake wanaopenda kusafisha sehemu zao za siri kwa kutumia sabuni zenye kemikali, marashi (manukato) au kupaka mafuta. Kwa maelezo ya wataalam, hao wapo hatarini kupata magonjwa ya zinaa au ya kuambukiza.
Sabuni ngumu au hata za maji, marashi (deodorant) zinaharibu tishu muhimu zilizomo ndani kabisa ya uke na kumweka mhusika katika hatari ya kupata malengelenge, na fangasi. Aidha, sabuni au dawa zinazouzwa na wafanyabiashara zikitangaza kuboresha uke au kuondoa harufu kwenye sehemu hizo nyeti nazo zimeelezwa kuwa na madhara.
Sabuni au mafuta yenye kemikali huchubua ngozi laini ya uke na ni rahisi vimelea vya magonjwa kuenea kwa urahisi. Michubuko hiyo ambayo si rahisi kuonekana kwa macho ndicho chanzo cha kuingia kwa maradhi ya kuambukiza.
Hakuna haja ya kuweka kemikali, au pafyumu ukeni. Hizo sehemu zinahitaji kuoshwa vizuri kwa maji safi ya baridi. Kemikali inapoingia ukeni inavuruga hali ya kawaida na asidi inayolinda sehemu hizo. Ni vyema wanawake wakaelimishwa kuhusu matumizi ya bidhaa zinazodaiwa kuweka harufu nzuri katika sehemu zao za siri, kurudisha bikira au mafuta ya kulainisha uke.
Wanawake wanaofanya usafi sehemu zao za siri kwa kutumia bidhaa au baadhi ya vifaa visivyofaa kutumiwa ukeni huweza kupata saratani ya shingo ya kizazi.Bidhaa zenye kemikali ya ‘coal tar,’ ambazo mara nyingine huwekwa kwenye sabuni ama manukato na kutumiwa ukeni na wanawake huweza kuchochea saratani hiyo.