Zifuatazo ni baadhi ya sababu hatarishi zinazochangia mimba kutunga nje ya kizazi ambazo ni;
1) Matatizo Katika Mirija Ya Uzazi
Matatizo kwenye mirija ya uzazi yanayoweza kusababisha mimba kutunga nje ya kizazi ni pamoja na;
Maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke (PID)
Matumizi ya vitanzi vya kuzuia mimba (Intra-uterine contraceptive devices)
Kuoteana kwa tishu za uterus kwenye viungo vingine vya uzazi au endometriosis.
Soma pia hii makala: Ujue Ugonjwa Wa PID(Pelvic Inflammatory Disease).
2) Uvutaji Sigara
Uvutaji sigara kwa mwanamke una uhusiano mkubwa na utungaji wa mimba nje ya kizazi. Imeonekana kwamba wanawake wanaopendelea kuvuta sigara mara kwa mara wana hatari ya kupatwa na tatizo hili mara tano zaidi ya wale wasiovuta kabisa. Hali hii husababishwa na nikotini iliyomo ndani ya sigara. Kwa kawaida nikotini huchochea kusinyaa kwa mirija ya uzazi hali iletayo kuziba kwa mirija hiyo na hivyo kufanya kiinitete kushindwa kupita kwenye mirija ya uzazi kuingia kwenye mji wa mimba na kufanya mimba kutunga nje kizazi.
3) Upasuaji Wa Tumbo Uliofanyika Zamani
Operesheni yeyote inayohusu mirija ya uzazi inaongeza uwezekano wa mimba kutunga nje ya kizazi kwa vile mirija ya uzazi huwa imesinyaa kutokana na operesheni hiyo.
4) Matumizi Holela Ya Baadhi Ya Dawa
Matumizi ya baadhi ya dawa zenye homoni husababisha kupungua kwa uwezo wa mirija ya uzazi kusukuma kiinitete kuelekea kwenye mji wa mimba na hivyo kuleta uwezekano wa utungaji wa mimba nje ya kizazi. Dawa hizo ni kama dawa za kuzuia mimba zenye homoni za kike za progesterone, na dawa za kusaidia uzazi aina ya clomiphene.
Kumbuka: Sababu zingine hatarishi zinazopelekea mimba kutunga nje ya kizazi ni pamoja na; Kutoa mimba zaidi ya 3, teknolojia saidizi za uzazi (assisted reproduction), umri wa zaidi ya miaka 35 kwa wanawake.