Kuongezeka kwa uzalishaji wa homoni ya progesterone wakati wa ujauzito kunafanya misuli ya mwilini kulegea. Hii inajumuisha pia misuli ya kwenye utumbo. Kulegea huku kwa misuli kunapunguza kasi ya mjongea wa chakula na hivo kupelekea choo kiwe kigumu au ukose choo.
Tatizo la kukosa choo na kupata choo kigumu kitaalamu(constipation) linawapata sana wajawazito wengi. Tafiti zinasema watatu kati ya wanne hupata tatizo hili na matatizo mengine kama kiungulia katika ujauzito wao.
Hatua 5 za Kutibu Kukosa Choo Wakati Wa Ujauzito
1. Kula zaidi vyakula vyenye kambakamba
Vyakula vyenye kambakamba vinafaa zaidi kuimarisha upatikanaji wa choo na pia vinaongeza vitamin na madini ya kutosha mwilini.
Vyakula hivi ni pamoja na mboga za majani, maharage, mapeas, mkate wa ngano isiyosafishwa(brown bread) ,ugali wa dona, ndizi na apple,mbegu za maboga, mihogo, karanga, magimbi na korosho.
2. Kunywa maji ya kutosha kila siku
Mjamzito anatakiwa kutumia maji mpaka glass 8 kwa siku. Hii itasaidia kulainisha choo na kusaidia usagaji mzuri wa chakula tumboni.
3. Kula kidogo kidogo walau mara 6 kwa siku
Usipende kula milo mikubwa mara tatu kama tulivyozoea. Jitahidi kugawanywa milo yako hata mara sita. Na usile ukashiba sana, kula kidogo kidogo mara nyingi. Kula chakula kingi kunapumguza kasi ya kusagwa chakula tumboni.
4. Fanya Mazoezi Madogomadogo
Mazoezi yanasaidia mwili kuchoma chakula haraka na kupunguza hatari ya chakula kubaki tumboni na hivo kukosa choo. Mazoezi yanachochea utolewaji wa choo. Wajawazito muhimu wafanye mazoezi mara tatu kwa wiki nusu saa kila siku.
Unaweza kuchagua kutembea, kuogelea au kufanya yoga. Zungumza na daktari kupata ushauri zaidi kuhusu mazoezi ya kukufaa.
5. Tumia Vidonge kulainisha Choo pale Inapobidi
Kabla ya kumeza dawa hakikisha umepata ushauri wa daktari. Kama umeshajaribu njia zote hizi imeshindikana basi kuna haja ya kupata vidonge vya kumeza.