Close

Close

Umuhimu wa Folic Acid kwa Mjamzito

Folic acid ni aina ya Vitamin B9. Ni muhimu kwa ukuaji wa uti wa mgongo, husaidia kuimarisha mifupa na ubongo wa mtoto akiwa tumboni. Ni muhimu sana mama mtarajiwa kutumia folic acid hasa wakati mimba ikiwa changa. Hii ni kwa sababu uti wa mgongo ndio moja ya sehemu za mwili ambazo hutengenezwa mapema kijusi kikiwa tumboni

Inashauriwa kila mwanamke ategemeaye kupata ujauzito atumie folic acid. Wanawake wenye miaka zaidi ya 14 wanahitajika kupata virutumisho vya folic acid kwa dozi ya microgramu 400 (mcg) kwa siku, na kiwango kiongezeke hadi microgramu 600 (mcg) wakati wa ujauzito. Na waendelee na microgramu 500 (mcg) kila siku wakati wa kunyonyesha.

Katika utafiti mmoja uliochapishwa katika jarida la kitabibu (PLOS) mnamo mwaka 2009, ulionyesha kuwa, wanawake waliotumia folic acid angalau miezi 12 kabla ya kupata ujauzito, walipunguza hatari ya kupata watoto walio njiti kwa asilimia 50 hadi 70.

Kazi za Folic Acid

  1. Folic acid ni muhimu katika utengenezwaji wa seli hai nyekundu za damu.
  2. Utengenezwaji na ukarabati DNA na RNA ambazo ni dutu muhimu za jeni.
  3. Husaidia mgawanyiko wa haraka wa seli hai katika mchakato wa ukuaji.
  4. Husaidia kuimarisha afya ya ubongo, hususan kwa ukuaji wa mtoto aliye tumboni.
  5. Husaidia kutuepusha na matatizo ya kusikia yatokanayo na umri mkubwa.
  6. Ni muhimu sana kwa wanawake walio wajawazito kutumia folic acid. Hii husaidia kuviepusha vijusi vilivyo tumboni dhidi ya ulemavu wa kuzaliwa kama wa ubongo au uti wa mgongo pamoja na kuwaepusha watoto na tatizo la mgongo wazi na kutokufunga kwa mfupa wa fuvu la kichwa (anencephaly).
  7. Kuzuia ugonjwa wa tawahudi (autism) umekuwa ukihusishwa na upungufu wa matumizi ya folic acid. Watoto wenye ugonjwa huu hawaonekani wenye tabia ya kawaida. Wakati mwingine hawapendi kuangalia wengine pale wanapozungumza nao, au hawapendi kushirikiana na watu wengine katika mambo kadhaa. Pia, hawapo vizuri katika mawasiliano. Muda mwingine huwa hawawezi kuongea au kuzungumza na watu wengine. Mwishoni, hujijibu wao wenyewe. Wanaweza wakawa na shauku na kitu ambacho mtu mwingine (ambaye hana tatizo la tawahudi) hafikirii kina umuhimu.
  8. Katika moja utafiti uliofanyika, umeonyesha kuwa matumizi ya folic acid na wajawazito huwaepusha watoto na mdomo sungura.

Vyakula vyenye folic acid kwa wingi.

Vyakula vyenye folic acid kwa wingi ni kama kiini cha yai, mboga za kijani za majani, Maini, Maziwa, Machungwa, Njegere, Alizeti, Mkate wa ngano isiyokobolewa. Na ni vyema kuepuka kupika katika joto kali na usitumie mafuta kwa kua hupunguza vitamini hii.

Wanawake wanaotegemea ujauzito ni vyema kutumia folic acid au kula vyakula vyenye vitamini hii kwa wingi mwaka mzima kabla ya kupata ujauzito ili kupunguza hatari ya mtoto kupata magonjwa tuliyoyaona hapo awali.